Friday, June 4, 2010

THE LIFE STYLE I BARE WITH

Tanzania, Msumbiji kubadilishana wanafunzi
News/Latest News
Author:abdullah al-talei
SERIKALI za Tanzania na Msumbiji zimekubaliana kubadilishana wanafunzi wa elimu ya juu na kwa kuanzia mwaka huu wanafunzi 50 kutoka pande zote watafaidika na mpango huo. Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Profesa Jumanne Maghembe juzi alitiliana saini makubaliano hayo na Waziri wa Elimu wa Msumbiji Zefarino Andrade de Alexandre Martins jijini Dar es Salaam. Profesa Maghembe alisema Watanzania watakaoenda kusoma nchini Msumbiji wataenda kujifunza lugha ya kireno, k ilimo, Sayansi, utamaduni na mambo ya uvuvi. “Tumeanza na idadi hii ya wanafunzi na kila mwaka sisi tutapeleka wanafunzi 50 na wao wataleta idadi hiyo hiyo katika vyuo vyetu hapa nchini, tunaweza kuongeza idadi kwa siku za baadaye,” alisema Maghembe. Hatua hiyo kwa mujibu wa Profesa Maghembe inatokana na ziara aliyoifanya Waziri Mkuu Mizengo Pinda nchini Msumbiji na kuzungumza na viongozi wa nchi hiyo kuona namna bora ya kushirikiana ili kuendeleza uhusiano uliopo baina ya nchi hizo mbili. “Moja ya mambo waliokubaliana ni kushirikiana kwa upande wa elimu, vijana wetu wa pande mbili watapata fursa ya kujifunza zaidi tamaduni za nchi hizi mbili zenye uhusiano wa kihistoria,” alisema Profesa Maghembe. Waziri huyo walimuhakikishia waziri huyo wa Msumbiji kuwa Tanzania imepiga hatua kubwa kwenye sekta ya elimu ya juu kutokana na idadi ya wanafunzi hao kuongezeka kila mwaka kutokana na idadi kubwa ya vyuo vilivyopo. Hata hivyo Waziri Maghembe alikiri mbele ya waziri huyo kuwa Tanzania kutokana na mapinduzi ya elimu ya juu na ile ya Sekondari, imejikuta inakuwa na upungufu mkubwa wa walimu, lakini akamwakikishia kuwa kutokana na ongezeko hilo la vyuo walimu watakuwa wengi katika siku zijazo. Naye waziri huyo wa Msumbiji alisema Tanzania imekuwa na uhusiano wa kihistoria na Msumbiji kabla ya uhuru na baada ya uhuru na hiyo inatokana na misingi iliyowekwa na waasisi wa mataifa hayo Mwalimu Julius Nyerere na Samora Machel. “Ni lazima nikiri kuwa Tanzania imetusaidia sana sisi Msumbiji hasa kijeshi katika kipindi cha harakati za kujikomboa na hata baada ya uhuru tumeendelea kushirikiana vizuri,” alisema Martins. Waziri huyo aliongeza kuwa wanatarajia vijana watakaokuja kusoma elimu ya juu hapa watakuja kujifunza Kiswahili na sekta nyingine yakiwemo mambo ya teknolojia ya mawasiliano (ICT), kilimo na uhandisi ili kuhakikisha nchi hiyo inafaidika na elimu inayotolewa na Tanzania. Alisema kuwepo mpango huo wa kubadilishana wanafunzi wa elimu ya juu ni kuendeleza mahusiano yaliyoasisiwa na wasisi na ndio maana wameona kuna haja ya watoto wa pande zote mbili kujifunzi lugha za pande zote mbili.

No comments:

Post a Comment