Katibu mkuu wa CCM, Yusuph Makamba, ameunganga na mwenyekiti wa chama chake kitaifa, aliye pia rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete, katika kututengenezea mwisho wa filamu ya kuchekesha yenye kuelezea matatizo ndani ya chama chao.
Wakati ambapo mheshimiwa JK, yeye alihitimisha kipande chake katika filamu hiyo akiwa jijini Dar es salaam, kwa staili ya kujibu maswali ya wananchi kupitia luningani, Makamba, yeye aliamua kumalizia kipande chake kule jimboni Urambo kwa staili ya kuhutubia wananchi kupitia mkutano wa hadhara.
Na kwakuwa kama zilivyo filamu zingine, hii nayo ilikuwa na script yake, bila shaka ndio maana haikuwa taabu kwa vigogo hawa kuwa na majibu ambayo yalishabihiana kwa karibu.Majibu ya kisanii.
Kwa Makamba ninayemjua, ambaye nimekuwa nikiamini kuwa anapoteza muda katika siasa ilhali tasnia ya sanaa ikiwa inamhitaji sana, hili lilikuwa jambo nililolitarajia. Ilikuwa suala la muda tu, ambao hatimaye aliupata na kuutumia vyema kama ilivyo ada kwake.
'Filamu' yenyewe ambayo sehemu kubwa ilichezwa mjini Dodoma, ilihusisha tukio linalomhusisha mtu mmoja ambaye kutokana na mapenzi yake kwa Watanzania wenzake, aliamua kusimama kidete katika upande wa kuwatetea.
Mhusika wa nafasi hii, Samwel 'a.k.a Standard and Speed' Sita, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambaye ni wazi kuwa amedhihirisha kasi na kiwango chake katika kulipa Bunge letu meno, alijikuta katika wakati mgumu kutokana na utendaji wake ambao kimsingi umekuwa ukizingatia ilani ya chama chake na kilicho pia chama tawala CCM.
Kuwaletea Watanzania maisha bora, kuimarisha mijadala yenye maslahi ya kitaifa ndani ya Bunge, kwa lengo la kuimarisha demokrasia, ni baadhi tu ya mambo yenye kuzungumzwa katika kila muongozo wa CCM, na ambayo Sitta, amekuwa akiyafanya.
Hata hivyo, ni mambo kama haya haya ambayo kada huyu mkongwe wa CCM, amekuwa akiyatekeleza kwa matendo, ambayo yalielekea kumponza.
Katika kile kilichoonekana kama kiashiria cha kiwango cha unafiki ulivyowajaa baadhi ya wana-CCM, na hususan watendaji wa ngazi za juu wa chama hicho, ilibakia almanusura Sitta, sio tu kuondolewa katika nafasi yake ya uspika bali pia kupokwa ubunge na uanachama wake katika CCM.
Taarifa za matukio haya yote zilikuwa wazi, ziliripotiwa na kusambaa kila kona ya nchi. Halikuwa kificho, lilikuwa jambo la wazi.
Kwamba baada ya vikao vile vya wakubwa kwisha hakukutolewa tamko lolote la kukanusha taarifa za kilichokuwa kimedhamiriwa kumkumba Sitta, ni ishara ya kuwa kweli kulikuwa na dhamira hiyo.
Tulimsikia Makamba, akiongea na vyombo vya habari, tena kwa lugha ya ukali, kuwa vikao hivyo vilikuwa na haki ya kufanya waliyoyafanya kwakuwa CCM ni zaidi ya kila mtu/kitu.
Kwamba CCM ni zaidi ya sheria za nchi, kwamba CCM ina haki ya kuvunja katiba ya nchi kwa kumhoji, kumdhalilisha na kutaka kumuwajibisha kiongozi mkuu wa mhimili wa nchi, kwa kutimiza wajibu wake ambao katiba ya nchi inamtaka kuutimiza.
Lakini katikati ya kiza kilichowashukia Watanzania juu ya uadilifu, uelewa, busara na utimilifu wa utendaji kazi walio nao viongozi na baadhi ya wana-CCM, wale waliostahili kuhakikisha unyoofu wa mambo, wakatujia na masimulizi ya kuvunja mbavu kwa vilio vya masikitiko.
Tukamsikia mwenyekiti wa CCM, mhe. Jakaya Kikwete, akituambia kuwa kilichojiri Dodoma, yalikuwa ni malumbano makali sana. Tukamsikia Makamba, akijinasibu kwa mama mzazi wa Spika wetu, kuwa hakuwa na matatizo na mh. Sitta.
Hakuna hata mmoja wao aliyetamka kuwa, taarifa za mzee wa viwango na kasi, alikuwa akizushiwa tu kuwa anataka kufukuzwa. Na hili linamaanisha kuwa ni kweli wana-CCM kupitia vikao vyao, walidhamiria kumtendea unyama huo.
Kwa Sitta, ambaye uadilifu wake kwa CCM, haujawahi kuwa jambo la kuhoji, kwa Sitta, ambaye mapenzi yake kwa CCM, yamemfanya aone kuwa chama kinaenda kubaya na kinahitaji kurejesha imani yake kwa wananchi na akaonyesha njia katika kurejesha imani hiyo, ni wazi kuwa yaliyotokea kule Dodoma, ulikuwa udhalilishaji mkubwa sana kwake.
Kwa mh. JK, kukaa kimya akaiachia hali ile akiwa ni mwenyekiti wa chama na akamnyamazia hata Makamba, aliyetoa kauli za kuhalalisha udhalilishaji ule, ni wazi kuwa, hata yeye alikuwa anayafurahia na kuyakubal.
Na kama mhe. JK, ameshindwa kuwakemea watu aina ya Makamba, ambao wanavunja katiba ya nchi kwa kuhoji utendaji wa Spika tenda ulio ndani ya muongozo sahihi kikatiba na kiilani ya CCM, ana sababu ipi ya kutufanya tuendelee kumuamini?
Hivi ikitokea Bunge nalo likaamua kumjadili raisi, kiasi cha kufikia kufikiri, angalau kufikiri tu, kuwa anatakiwa aondoke madarakani, atakaa kimya na kuyachekelea hayo?
Hapa ndipo ninapokumbuka alichowahi kuandika Ansbert Ngurumo, kuwa mh JK, ni kama mtu ambaye hawezi hata kuchinja kuku wake, kwakuwa anaogopa kurukiwa na damu, kwahiyo atatafuta mtu amsukumie mzigo huo.
Na hili ndilo alilolitenda kwa kuunda tume ya kuchunguza kiini cha malumbano baina ya wabunge wa CCM. Ilikuwepo haja gani ya kufikia hapo, ilhali inajulikana wazi kuwa ni ukosefu wa msukumo wa kweli, wazi na ulio wa haraka katika kushughulikia matatizo ya wazi ya wananchi!
TAARIFA HII NIMEITOA KATIKA BLOG YA Rama Msangi
• Age: 34
• Gender: Male
• Astrological Sign: Virgo
• Zodiac Year: Rabbit
• Industry: Publishing
• Occupation: Journalist
• Location: Mbeya : Southern Highland Zone : Tanzania
www.uchambuzi.blogspot.com
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment